Rais William Ruto ameagiza kutwaliwa tena kwa ardhi ya serikali inayodaiwa kunyakuliwa katika Kaunti ya Kiambu.
Akiongea leo Jumamosi alipozindua ujenzi wa barabara ya Thika-Magumu, eneo la Gatundu Kaskazini, Rais Ruto aliagiza mashirika husika kuhakikisha ardhi yote ya Serikali iliyonyakuliwa inarejeshwa, ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbali-mbali ya serikali ukiwamo ule ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na ujenzi wa masoko ya kisasa, miongoni mwa miradi mingine.
Aliahidi kuzindua ujenzi wa nyumba 10,000 za gharama nafuu katika Kaunti ya Kiambu, mwezi Disemba, mwaka huu.
Aidha, kiongozi wa taifa alisema, atazindua ukarabati wa barabara za miji kwa ushirikiano wa serikali za Kaunti kujenga masoko 20 mapya ya kisasa.
Rais alimwagiza waziri wa maji, Alice Wahome kushughulikia swala la uhaba wa maji katika eneo hilo katika muda wa majuma mawili yajayo.
Kwa upande wake, Naibu Rais, Rigathi Gachagua aliitetea serikali kuhusiana na bei za juu za mafuta, akisema kuwa hilo ni tatizo la Kimataifa.
Alitoa wito wa kudumishwa kwa subira huku serikali ikitekeleza marekebisho katika sekta ya kahawa.