Serikali imepiga marufuku uagizaji mahindi na ngano kutoka mataifa ya nje, katika hatua iliyotajwa ya kuwakinga wakulima wa hapa nchini.
Rais William Ruto alisema haitatoa leseni za kwa kampuni za kusaga unga kuagiza nafaka hizo kutoka nje, akidokeza kuwa agizo hilo litabatilishwa iwapo mazao ya humu nchini hayatatosha.
Aidha kiongozi wa taifa alisema serikali itatenga shilingi bilioni nne kununua mahindi kutoka kwa wakulima, akidokeza kuwa hatua hiyo inalenga kuthibiti bei ya bidhaa hiyo.
Akizungumza Alhamisi katika ikulu ya Nairobi, alipokutana na ujumbe kutoka eneo bunge la Narok kaskazini ukiongozwa na mbunge wa eneo hilo Agnes Pareiyo, Rais Ruto alitangaza kwamba mitambo ya ukaushaji ya halmashauri ya nafaka na mazao hapa nchini NCPB, itatumiwa kukausha mahindi ya wakulima kwa ada ya shilingi 50 katika juhudi za kupunguza hasara ya baada ya mavuno kutokana na kiwango cha juu cha unyevunyevu.
“Tunatoa wito kwa wakulima wasiuze mahindi kwa bei iliyodhoofika,”alisema Rais.
“Ikiwa wakulima hawataki kuuza mahindi yao kwa NCPB, watakuwa na nafasi ya kukausha mahindi yao katika ghala hilo la serikali,”alieleza Rais.
Wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu na mwenzake wa Samburu Jonathan Leleliit, mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo, wawakilishi wadi na viongozi wa mashinani.