Rais Ruto apendekeza kubuniwa kwa taifa la Palestina

Tom Mathinji
1 Min Read

Rais William Ruto amependekeza kubuniwa kwa mataifa mawili ya Israel na Palestina, ili kusitisha mzozo unaoshuhudiwa katika eneo la Gaza.

Kiongozi wa taifa aliyasema hayo Alhamisi jioni, alipojadiliana Kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu mzozo wa Gaza.

Kiongozi wa taifa alielezea hisia za Kenya kuhusu hali ilivyo katika eneo hilo, hasa kuhusiana na idadi kubwa ya vifo vinavyoripotiwa kwenye mzozo huo.

Rais Ruto pia alikariri msimamo wa Kenya dhidi ya ugaidi akisema uovuo huo lazima ukabiliwe.

Israel ilianza mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika eneo la Gaza, baada ya wapiganaji hao kutekeleza mashambulizi dhidi ya Israel tarehe saba mwezi Oktoba mwaka 2023.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, vita hivyo vimesababisha watu milioni 1.7 kutoroka makwao, hii ikiwa ni asilimia 80 ya wakazi wa Gaza.

Share This Article