Rais William Ruto amesema hawezi kukubalia watu wachache waharibu hali ya baadaye ya nchi hii kwa hivyo ufisadi utakabiliwa vilivyo.
Kiongozi wa nchi ambaye alikuwa akizungumza kwenye Ikulu Ndogo ya Kakamega kwenye mkutano na viongozi wa kaunti za Kisii, Nyamira na Migori, alisema watu wachache ambao wanahujumu miradi ya maendeleo nchini hawatavumiliwa.
Alionya wafisadi kwamba sasa hawataweza kijificha kwenye mahakama na maagizo kutoka kwa mahakama kwani serikali itashirikiana na idara ya mahakama kuondoa watu ambao wana mitazamo hasi kazini.
Viongozi waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, Magavana Simba Arati wa Kisii na Amos Nyaribo wa Nyamira, wabunge, wawakilishi wadi na viongozi wengine wengi wa mashinani. Wote walikubali kushirikiana na serikali kubadilisha Kenya.
Rais alisihi viongozi hao wasiangazie tu maslahi ya vyama vyao ambayo huenda yakalemaza maendeleo nchini, huku akiwakumbusha kwamba wakati wa kampeni kila mmoja aliahidi kufanyia wananchi kazi na sasa wana fursa ya kufanya hivyo.
Kulingana na kiongozi wa nchi, ahadi zilizotolewa kwa Wakenya zinaweza kutekelezwa iwapo viongozi wataungana.