Rais Ruto ameondoka nchini Jumapili jioni kwa ziara rasmi ya kiserikali nchini Marekani anakotarajiwa kusaini mikataba kadhaa ya ushirikiano katika sekta mbali mbali.
Ruto ataanza ziara yake Jumatatu kwa kuzuru Atlanta, Georgia atakapotembelea makavazi na maktaba ya Kirais.
Rais pia atazuru kanisa la Ebenezer Baptist kutoa heshima kwa wapiganiaji wa haki za kibinadamu waliouawa.
Kwenye ziara yake nchini Marekani Rais Ruto pia anatarajiwa kusaini mikataba kadhaa katika kituo cha kudhibiti maradhi yaani CDC .
Siku ya Jumanne Rais atazuru chuo cha Spelman atakapojadili mchango mhimu wa vyuo na pia mchango wa Kenya katika maendeleo ya nguvukazi na baadaye kuzuru studio za Tyler Perry kubaini fursa za ushirkiano katika sekta ya sanaa na kutembelea pia makao makuu ya kiwanda cha Coca Cola ambapo mkataba mpya wa ushirikiano unatarajiwa kutangazwa.
Baadaye Jumanne Rais atalakiwa na Meya wa Atlanta kando na kufungua duka la Vivo la Kenya linalouza nguo nchini Marekani.
Jumatano Ruto na mkewe watawasili mjini Washington D.C’s ambapo watapokea makaribisho rasmi ya kiserikali,kabla ya kuhutubia mabunge yote mawili
Alhamisi Rais Ruto atafanya kikao na mwenyeji wake Joe biden kujadiliana kuhusu mikataba kadhaa ya ushirikiano baina ya nchini hizo mbili, kabla ya kutoa hotuba kwenye ikulu ya White House.
Siku ya Ijumaa Ruto atafanya mazungumzo na makamu Rais wa Marekani Kamala Harris, kabla ya kuzuru Pentagon ambapo atajadiliana kuhusu ushirikiano katika sekta ya ulinzi na vita dhidi ya ugaidi.