Rais William Ruto ameungana na viongozi wengine duniani kuomboleza kifo cha Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter.
Carter, ambaye aliapishwa kuchukua madaraka kama Rais wa Marekani Januari 20, 1977, amefariki akiwa na umri wa miaka 100.
Alikuwa Rais wa 39 wa Marekani.
“Rais Jimmy Carter alikuwa kiongozi asiyekuwa wa kawaida ambaye kujitolea kwake kuhudumia umma kulikuwa kwa kishujaa. Alikuwa mpiganiaji shupavu wa kupatikana kwa amani na haki za binadamu duniani,” amesema Rais Ruto katika rambirambi zake.
“Tunashukuru kutokana na sauti yake anzilishi kwa vitendo vya dunia nzuri ambayo imelinda mazingira yetu na kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabia nchi.”
Rais Ruto ameelezea kuwa kwa sasa anaiombea familia ya Carter na watu wa Marekani wakati huu wa maombolezi.
Kifo cha Rais Carter kilithibitishwa na kituo cha Carter Centre alichoanzisha na ambacho hutetea demokrasia na haki za binadamu kote duniani.
Kituo hicho kilisema Rais Carter alifariki jana Jumapili mchana akiwa nyumbani kwake huko Plains, Georgia.
Rais Carter alihudumu kati ya mwaka 1977 hadi 1981, kipindi ambacho kilikumbwa na migogoro ya kiuchumi na kidiplomasia.