Rais Ruto amwomboleza Binti ya Seneta Mungatana

Kulingana na familia kitindamimba huyo alifariki Jumapili, Septemba 13, 2026, akipokea matibabu.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ametuma salamu zake za rambirambi kwa Seneta wa Tana River, Danson Mungatana, na mkewe, Naibu Msemaji wa Serikali, Mwanaisha Chidzuga.

Haya yanafuatia kifo cha binti yao wa miaka minane, Amal Mghoi Mungatana.

Katika ujumbe aliochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Rais Ruto alielezea kifo cha Amal kuwa hasara ya ghafla na kutoa pole kwa familia, marafiki na wote waliomfahamu na kumpenda mtoto huyo.

“Kuondokewa na mtoto ni huzuni isiyo na kifani,” Ruto alisema, huku akimwomba Mungu kuipa familia nguvu, faraja na amani katika kipindi hiki kigumu.

Familia ilitangaza kuwa Amal, ambaye alikuwa mtoto wao wa mwisho, alifariki Jumapili, Septemba 13, 2026, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Watoto ya Gertrude’s, Muthaiga, Nairobi.

Kwa mujibu wa tangazo la kifo, Amal alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya tangu alipozaliwa na alipatiwa matibabu nchini Kenya na nje ya nchi katika kipindi cha miaka yake minane.

Familia ilisema inamshukuru Mungu kwa furaha, tabasamu na upendo ambao Amal aliwaletea kila mara afya yake ilipokuwa ina matatizo.

Familia kwa sasa ianafanya mikutano katika makazi yao ya Kijiji cha Ngao, Kaunti ya Tana River, huku maandalizi ya mazishi yakiendelea.

Amal anatarajiwa kuzikwa Ijumaa, Septemba 18, 2026 Kijijini Ngao.

Ruto alihitimisha ujumbe wake kwa kuiombea roho ya Amal ipumzike kwa amani ya milele.

Share This Article