Rais Ruto ampongeza Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Keir Starmer

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Keir Starmer.

Rais William Ruto amempongeza Waziri Mkuu mpya wa Uingereza  Keir Starmer, kufuatia ushindi wake katika  Uchaguzi Mkuu nchini humo.

Kwenye taarifa katika mtandao wa  X, rais aliutaja ushindi wa  Starmer kuwa ishara ya azma kubwa ya raia wa Uingereza ya kutaka siasa za maendeleo na sera mwafaka za chama cha  Labour.

“Kwa niaba ya serikali na raia wa Kenya, nampongeza Keir Starmer baada ya uungwaji mkono wa chama cha  Labour katika Uchaguzi Mkuu uliopita, na kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza,” alisema Rais Ruto Jumamosi asubuhi.

Rais Ruto alisema atashirikiana kwa karibu na Waziri huyo Mkuu wa Uingereza,  ili kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili kwa manufaa ya raia wa mataifa hayo.

“Nitashirikiana na Waziri Mkuu Starmer kukuza biashara, ulinzi, siasa na kujenga mustakabali salama ulio na usawa na endelevu,” aliongeza kiongozi wa nchi.

Starmer aliongoza chama cha  Labour kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi ulioandaliwa siku ya Alhamisi nchini humo na kuhitimisha utawala wa miaka 14 wa chama cha Conservative.

Kuteuliwa kwake kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kulitangazwa rasmi katika ikulu ya  Buckingham siku ya Ijumaa, alipokutana na mfalme  Charles wa Tatu.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *