Rais Ruto alalamikia pepo wa kupinga kila kitu miongoni mwa Wakenya

Martin Mwanje
3 Min Read

Rais William Ruto amelalamikia vikali kile ambacho amekiita kuwa pepo wa kupinga kila kitu miongoni mwa Wakenya. 

Alielezea lalama zake wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuchakata chuma wa kiwanda cha Devki katika eneo la Manga, kaunti ya Taita Taveta.

“Na mimi nataka niwaulize Wakenya. Tafadhalini, kuna pepo chafu ya upingamizi, kupinga kila kitu. Kiwanda kama hii, watu wanaipinga. Affordable Housing, wanaipinga. Chanjo ya ng’ombe kuondoa magonjwa, wanaipinga. Kubadilisha mfumo ndio tuweze kuokoa universities zetu ambazo zilikuwa zinakwama, wanaipinga,” alilalama Rais Ruto katika hatua ambayo iliiacha hadhira ikivunjika mbavu kwa cheko kubwa.

“Kupinga hata miradi yoyote ya serikali. Mambo ya Universal Health Coverage, wanaipinga. Mambo ya afya, wanaipinga. Sasa mimi nauliza, hii pepo chafu, nafikiri imefika wanapinga hata matoleo kanisani. Jamani?”

Lalama za Rais Ruto zinakuja wakati ambapo Wakenya wamekuwa mstari wa mbele kupinga maamuzi ya serikali ya Kenya Kwanza wanayodhani ama ni kandamizi au yamekusudia kubadhiri rasilimali za umma.

Pingamizi zao zilianzia hususan kwa Mswada wa Fedha 2024, mswada ambao ulikuwa chimbuko la maandamano ya vijana wa Gen Z mwezi Juni mwaka huu. Maandamano hayo yalichochea kufutiliwa mbali kwa mswada huo lakini baada ya watu kadhaa kufariki na wengine wengi kujeruhiwa.

Bima ya Afya ya Jamii ya SHIF pia imekumbana na shutuma kutoka kwa Wakenya wanaolalamikia matozo ya hali ya juu wakati kumekuwa na changamoto tele katika upataji huduma. Serikali imeahidi kushughulikia changamoto hizo huku Rais Ruto akielezea imani kuwa mpango huo utaleta usawa katika upatikanaji wa huduma za afya miongoni mwa Wakenya.

Aidha, mpango wa nyumba za gharama nafuu umekosolewa na Wakenya wanaouchukulia kuwa njama ya utawala wa sasa kuwapunja fedha zao wakati hawana hakikisho la kupata nyumba hizo.

Pingamizi za hivi punde kutoka kwa Wakenya zilihusu makubaliano ya Adani yaliyokusudia kustawisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA na pia kujenga laini za usambazaji umeme nchini. Ni pingamizi zilizosababisha Rais Ruto kutangaza kufutiliwa mbali kwa makubaliano hayo.

Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka naye amewaongoza viongozi wengine wa upinzani kupinga mpango wa kutoa chanjo kwa mifugo uliokusudiwa kuanza mwezi Januari mwaka ujao. Kalonzo na wenzake wameonekana kutilia shaka usalama wa chanjo hiyo.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *