Rais Ruto alalamikia wanaotumia mahakama kuhujumu serikali

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto ameelezea wasiwasi kuhusu kile alichokitaja kuwa hatua ya watu fulani kutumia vibaya mahakama kuhujumu mipango ya serikali.

Rais alisema watu hao wameteka maafisa fulani wa mahakama ili kulemaza juhudi za serikali za kuzuia wizi wa raslimali za umma.

Kulingana naye haina maana kwa watu wachache kuafikia matakwa yao huku umma ukiteseka.

Kiongozi wa nchi aliitaka idara ya mahakama ijitolee kufuata katiba na kuhudumia Wakenya.

“Tutalinda uhuru wa mahakama. Lakini hatutakubalia watu wachache wenye nia mbaya kuiteka,” alisema Rais.

Rais aliyasema hayo Jumanne Januari 2, 2024 huko Njambini kaunti ya Nyandarua wakati wa mazishi ya baba ya seneta John Methu, Mzee Michael Maigo Waweru.

Alimtaja marehemu Mzee Waweru kuwa mtu aliyejitolea kuhudumia Jamii, aliyeheshimika, kiongozi wa ujasiriamali na ambaye alikuwa na mawazo mazuri yaliyobadilisha maisha ya wengi.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ya mazishi ni pamoja na Naibu Rais Rigathi Gachagua, waziri Rebecca Miano, Spika wa Seneti Amason Kingi, Gavana wa Nyandarua Kiarie Badilisha na wabunge kadhaa wakiongozwa na kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah pamoja na wawakilishi wadi.

Share This Article