Rais Ruto akutana na wabunge waliofurushwa na chama cha ODM

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto akutana na wabunge wa ODM waliofurushwa. Picha Hisani.

Siku moja baada ya chama cha ODM kuwatimua baadhi ya wabunge wake wanaoshtumiwa kuegemea upande wa serikali, Rais William alishiriki meza ya mazungumzo na wabunge hao  katika Ikulu ya Nairobi, huku wabunge hao wakiahidi kuendelea kushirikiana na serikali.

Wabunge hao waliofurushwa na chama cha ODM ambao ni pamoja na mbunge wa Gem Elisha Odhiambo, Seneta wa Kisumu Tom Ojienda na mbunge wa Lang’ata Felix ‘Jalang’o’ Odiwuor, walipongeza hatua ya serikali ya kushughulikia ipasavyo changamoto zinazoghubika sekta ya sukari hapa nchini.

Wakati wa mkutano huo wa siku ya Jumatano, wabunge hao waliahidi kuunga mkono mswada wa sukari utakapowasilishwa bungeni kujadiliwa siku ya Alhamisi.

Aidha walimualika rais kuzuru eneo la Nyanza kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.

Hata hivyo wabunge hao wa ODM walipata afueni ya muda baada ya jopo la kusuluhisha mizozo ya vyama vya kisiasa,  kusitisha kutimuliwa kwao chamani.

Mwenyekiti wa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa Desma Nungo, alitoa maagizo ya kukizuia chama cha ODM kutekeleza uamuzi wa kuwaondoa chamani wabunge hao hadi kesi iliyowasilishwa kupinga uamuzi huo itakaposikizwa na kuamuliwa.

Share This Article