Rais William Ruto leo Ijumaa amekutana na Maaskofu wa Kanisa Katoliki katika Ikulu ya Nairobi.
Rais Ruto amepongeza dhamira ya Kanisa Katoliki kushiriki mazungumzo yatakayoleta pamoja sekta mbalimbali ili kutafuta suluhu kwa masuala mbalimbali yanayolikumba taifa.
“Kupitia mtazamo huu wa pamoja, tutaisongesha Kenya mbele,” alisema Rais Ruto alipokutana na Maaskofu hao walioongozwa na mweyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini, KCCB Maurice Muhatia.
Mkutano huo unakuja siku chache baada ya Maaskofu hao kupinga Mswada tata wa Fedha 2024 ambao sasa umefutiliwa mbali.
Katika kuchukua hatua hiyo, Maaskofu hao walisema ikiwa mswada huo ungepitishwa jinsi ulivyokuwa, basi ungewakandamiza Wakenya.
“Ni mtazamo wetu kwamba Mswada wa Fedha 2024, ikiwa utapitishwa jinsi ulivyo, utakuwa kandamizi na kusababisha mateso yasiyoelezeka kwa Wakenya,” awali walionya katika taarifa.
“Ingawa tunafahamu kuwa serikali ina wajibu wa kukusanya kodi ili kufadhili huduma za umma, tuna mashaka mno kuhusu baadhi ya mapendekezo kwenye mswada huo yanayolenga kuongeza ukusanyaji wa mapato. Isitoshe, tunahuzunika juu ya ufisadi uliokithiri katika taasisi zetu za umma na ubadhirifu wa rasilimali za umma kwa shughuli zisizokuwa muhimu.”
Yamkini hizo ni baadhi ya shinikizo zilizomlazimu Rais Ruto kuamua kuondoa mswada huo mbali na maandamano ya vijana wa Gen Z yaliyoandaliwa kote nchini kuupinga.
Rais Ruto ameelezea nia ya kufanya mazungumzo na vijana hao pamoja na viongozi wa kidini, mashirika ya kijamii na washikadau mbalimbali ili kuangazia changamoto zinazolikumba taifa hili.