Rais Ruto akariri kujitolea kwa serikali kuunga mkono biashara ndogo

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesema serikali yake imejitolea kuunga mkono biashara ndogo na za kadiri kama njia ya kupanua wigo wa fursa kwa Wakenya na hatimaye kutokomeza tatizo la ukosefu wa ajira na umaskini.

Akizungumza katika kituo cha magari ya uchukuzi cha Green Park jijini Nairobi wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa hazina ya Hustler, kiongozi wa nchi alisema kila mwaka, serikali itatenga shilingi bilioni 12 ili wanabiashara wapate mikopo bila riba.

Ruto alisema kufikia sasa, serikali imedhibiti uchumi wa nchi na kuanzia mwezi Disemba mwaka huu, serikali itaanza kulipa madeni yake.

“Mwaka mmoja uliopita, tulikuwa katika hali mbaya kiuchumi ya kushindwa kuwajibikia madeni yetu, lakini kwa sababu ya maamuzi ambayo tumefanya katika muda wa mwaka mmoja uliopita, leo hii ninaweza kuhakikishia taifa kwamba Kenya sasa iko katika mwelekeo mzuri kiuchumi,” alisema kiongozi wa nchi.

Kuhusu gharama ya maisha, Rais Ruto alisema hatua ambazo wamechukua katika kusuluhisha hilo zimeanza kuzaa matunda. Alitaja kushuka kwa bei ya pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi ambayo alisema sasa ni shilingi 140.

Kufikia sasa, hazina ya Hustler imetoa mikopo ya karibu shilingi bilioni 40 ilhali ilianza na shilingi bilioni 12 pekee.

Wakenya kadhaa ambao wamefaidika kutokana na hazina ya Hustler walipata fursa ya kuonyesha biashara zao huku wengine wakisimulia jinsi walianza kukopa na walipofikia hadi sasa.

Maadhimisho ya mwaka mmoja wa hazina ya Hustler yalihudhuriwa pia na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo Simon Kiprono Chelugui, na Naibu Gavana wa kaunti ya Nairobi Njoroge Muchiri kati ya wengine.

Share This Article