Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Bomas utakapokamilika, utaiweka Nairobi kama kitovu kikuu cha mikutano mikuu na maonyesho barani Afrika, hayo ni kwa mujibu wa Rais William Ruto.
Akizungumza alipokagua ujenzi unaoendelea wa ukumbi huo siku ya Ijumaa, kiongozi wa nchi alidokeza kuwa ukumbi huo wa kisasa umeundwa kuwavutia wajumbe wa kimataifa na kuimarisha hadhi ya Kenya katika maswala ya utalii na kuandaa mikutano ya kimataifa.
“Maelfu ya wajumbe watakutana hapa na hivyo kuimarisha hadhi ya Kenya katika Utalii na kuwa mwenyeji wa mikutano ya kimataifa,’ alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa taifa alidokeza kuwa ukumbi huo pia utajumuisha maduka, hoteli tatu hivyo kufanikisha hafla za kimataifa na biashara za kitalii.

“Ujenzi wake utakapokamilika, ukumbi huu utakuwakimu wajumbe 11,000 kwenye vyumba 35 vya mikutano huku ukumbi mkuu ukiwakimu wajumbe 3,000,” aliongeza Rais Ruto.
Aidha kiongozi wa nchi alisema ameridhishwa na ujenzi unaoendelea wa ukumbi huo.
Wafanyakazi 2,500 wanashiriki ujenzi wa ukumbi huo.