Rais William Ruto ameelezea haja ya ushirikiano miongoni mwa wakenya ili kuafikia maendeleo ya taifa hili.
Akizungumza jana wakati wa ibada ya Jumapili Dagoretti kaunti ya Nairobi, Rais Ruto alitetea ushirikishwaji wa serikali jumuishi akiongeza kuwa unaiwezesha serikali kuafikia matakwa ya wakenya wote.
Rais Ruto alikariri haja ya kuzingatiwa kwa suala la umoja nchini akisema ni muhimu katika kuendeleza ustawi wa kiuchumi wa nchi hii.
Wakati uo huo, Rais Ruto alisema serikali itaimarisha hadhi ya jiji la Nairobi kama jiji kuu la nchi ili kukweza kiwango chake katika masuala ya kijamii na kiuchumi.
Rais Ruto alisema jiji la Nairobi ndilo jiji kuu hivyo basi ipo haja ya kulishughulikia kuafiki kiwango kinachofaa.
Wakati huo huo Rais William Ruto amewaomba wakenya kumuunga mkono aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa tume ya muungano wa bara Afrika (AUC) mwezi ujao.
Rais Ruto alitoa wito kwa taifa kumuunga mkono Raila, akisema kwamba ushindi wake utalifaa taifa hili pakubwa, akisema wanaompinga Raila kuwania wadhifa huo, wanafaa kusitisha shutuma zao na badala yake kuimarisha umoja na kumtakia kila la kheri
Raila ameonyesha nia na ari ya kushinda wadhifa huo, na amesisistiza kwamba kinyang’anyiro hicho kwa kawaida kina mshindi na mshinde.
Uchaguzi wa wadhifa huo uitafanyika mwezi Februari huku mwenyekiti wake kwa sasa Moussa Faki raia wa Chad akijiandaa kuondoka baada ya kipindi chake cha mihula miwili kukamilika.