Rais William Ruto amehakikishia maafisa wa usalama uungwaji mkono, akisema kwamba mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi huenda yakachochea machafuko na hayawezi kuvumiliwa.
Rais alikuwa akizungumza jana katika ikulu ya Nairobi alipokuwa mwenyeji wa wa maafisa wa usalama wa kimaeneo na kaunti pamoja na maafisa wa utawala wa serikali kuu.
Alitoa hakikisho kwamba serikali yake itasimama na kila afisa wa usalama awe wa kike au wa kiume na kuwalinda wanapoendelea kutekeleza majukumu yao.
Kiongozi huyo wa nchi alisema kwamba kamwe hakuwezi kuwa na nchi ambapo wahalifu wanakimbiza maafisa wa usalama na kuhatarisha maisha yao akiongeza kusema kwamba mtindo huo ni lazima ukomeshwe.
Rais Ruto alisema kwamba wahalifu waliovamia maafisa wa polisi na kuharibu mali wakati wa maandamano ya siku ya Jumatano, watawajibishwa.
Rais alisema kwa kulinda maafisa wa usalama, wakenya watakuwa na nchi thabiti yenye ulinzi ambapo maendeleo ya maana yanaweza kuafikiwa.
Matamshi ya kiongozi wa nchi yanafuatia matukio ya Jumatano ambapo maafisa wa usalama walionekana kuzidiwa nguvu na wananchi katika maeneo mbali mbali na ripoti za kuchomwa kwa vituo vya polisi.
 
					 
				 
			
 
                                
                              
		 
		 
		 
		