Rais William Ruto leo Jumatatu amefanya ziara ya ghafla katika ghala ya Halmashauri ya Nafaka na Mazao, NCPB mjini Eldoret.
Katika ziara hiyo, Rais Ruto alitoa agizo kwa usimamizi wa NCPB kote nchini kuharakisha usambazaji wa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima, huku akidokeza kuwa wanaouza mbolea bandia watachukuliwa hatua za kisheria.
Ziara hiyo ya Rais inajiri muda mfupi baada ya maafisa wa upelelezi wa jinai, DCI kuwataka maafisa kadhaa wa idara za serikali wanaohusika na usambazaji wa mbolea bandia kufika mbele yao ili kuhojiwa.
Kundi la kwanza lilihojiwa kuanzia siku ya Ijumaa hadi jana Jumapili, lililojumisha wawakilishi kutoka shirika la kukadiria ubora wa bidhaa KEBS na wasambazaji.
Wale kutoka halmashauri ya NCPB, wanatarajiwa kuhojiwa na maafisa wa upelelzi wa maswala ya jinai DCI, leo Jumatatu April 8.
Kulingana na maafisa, wale wote waliohusika na ununuzi na usambazaji wa mbolea hiyo feki watahojiwa.