Rais Ruto aendesha gari linalotumia umeme Nairobi

Marion Bosire
1 Min Read

Jumapili Septemba 3 2023, Rais William Ruto alijiendesha mwenyewe kwenye gari linalotumia umeme kutoka Ikulu ya Nairobi hadi jumba la KICC kuhudhuria mkutano wa vijana wa Bara Afrika kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Kiongozi wa nchi alikuwa na abiria mmoja kwenye gari hilo dogo la rangi ya samawati la kampuni ya Autopax AirEv YETU na msafara wake pia ulikuwa wa magari madogo yanayotumia nguvu za umeme kinyume na magari makubwa yanayotumia mafuta ambayo huwa anatumia kwa kawaida.

Anahisi magari hayo ndiyo yanafaa siku zijazo katika juhudi za kuafikia matumizi ya kawi isiyochafua mazingira.

Serikali yake imekuwa ikiendeleza mipango ya kuhakikisha matumizi ya nishati mbadala na vyombo vya uchukuzi visivyochangia uchafuzi wa mazingira.

Ijumaa alizindua pikipiki zinazotumia nguvu za umeme katika bustani ya Mama Ngina Waterfront mjini Mombasa na waongoza msafara wa rais leo walitumia pikipiki hizo za umeme.

Mwezi Juni mwaka huu, kampuni ya Autopax ya Kenya ambayo ndiyo ya kwanza kabisa ya kuunda magari yanayotumia nguvu za umeme nchini ilitangaza kwamba imeingia kwenye mapatano na kampuni moja ya kimataifa ya kuunda magari mapatano yakiangazia uundaji wa magari ya umeme oyatakayouzwa na kutumika nchini.

Share This Article