Rais William Ruto amewatakia Wakenya heri ya Mwaka Mpya na kuelezea matumaini kuwa 2025 utakuwa mwaka ambao Kenya itaendelea kufikia upeo wa maendeleo.
Akihutubia taifa kutoka kaunti ya Kisii, Rais Ruto alikiri kuwa mwaka 2024 ulikuwa na changamoto nyingi zilizofanya hali ya maisha kuwa ngumu kwa Wakenya wengi.
Hata hivyo, serikali yake iliweka mikakati ambayo imehakikisha Kenya inaibuka kuwa thabiti kiuchumi.
“Leo, tumefanikiwa kuwekaa msingi thabiti wa hata maendeleo ya kasi mwaka ujao. Sarafu ya Kenya, iliyoanza mwaka kwa kuyumba, imeimarika pakubwa, ikiimarika kutoka shilingi shilingi 165 dhidi ya dola mwezi Februari 2024 hadi shilingi 129 hii leo, na kuifanywa kuwa miongoni mwa sarafu zinazofanya vyema zaidi duniani,” alisema Rais Ruto.
“Mfumko wa bei, kiashiria kikuu cha ukuaji wa uchumi, umepungua kutoka asilimia asilimia 9.6 mwezi Septemba mwaka 2022 hadi asilimia 2.7 mwezi Oktoba 2024, kiwango cha chini zaidi katika karibu kipindi cha miongo miwili.”
Rais pia aliongeza kuwa uchumi wa nchi unaendelea kukua kwa kasi, kiasi kwamba mwaka jana, ulikua kwa asimilia 5.6.
Kuhusiana na mpango tata wa utoaji chanjo kwa mifugo, Rais amesema mpango huo utakuwa wa hiari na kuwahakikishia wakulima kuwa unakusudia kuhakikisha mifugo wanakuwa na kinga dhidi ya maradhi na hivyo kuongeza soko la mifugo hao duniani.
Aidha, aligusia mipango mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza kama vile utoaji wa mbolea ya bei nafuu na Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA, mipango ambayo alisema imekusudia kubadili dira ya nchi kimaendeleo.