Rais Ruto aelekea Roma Italia kwa ziara rasmi

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto ameondoka nchini kwa ziara rasmi huko Roma Italia ambako anatarajiwa kuhudhuria kongamano la Italia na Afrika.

Lengo kuu la kongamano hilo la siku mbili ni kuboresha uhusiano kati ya Italia na bara Afrika.

Litatumiwa pia kuweka wazi mpango makhsusi wa taifa la Italia unaolenga kubadili jinsi imekuwa ikihusiana na bara hili.

Nyanja mbali mbali za ushirikiano zitazungumziwa kwenye kongamano hilo kama vile kujitosheleza kwa chakula, utamaduni, elimu, elimu ya kiufundi, usalama wa kawi, uchumi na maendeleo ya miundomsingi.

Ushirikiano katika kukabiliana na ulanguzi wa binadamu na ugaidi vitajadiliwa pia kwenye kongamano hilo.

Rais Ruto katika wadhifa wake kama mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa nchi za Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi atahutubia kongamano hilo.

Amatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais Sergio Mattarella wa Italia ambapo watadurusu mapatano yaliyoafikiwa Rais Mattarella alipozuru Kenya na katika mikutano ya awali na waziri mkuu Giorgia Meloni.

Mpango huo makhsusi wa Italia kuhusu Afrika umepatiwa jina la Mattei. Miaka ya 1950 Enrico Mattei alitetea sana hatua ya Italia kufadhili nchi za Kaskazini mwa Afrika ili kukuza chumi zao na raslimali.

Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni ndiye anasukuma mpango huo utakaogharimu Yuro milioni 3 Kila mwaka na utatekelezwa kwa miaka minne.

Share This Article