Rais Ruto achukua uenyekiti wa COMESA

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akikabidhiwa mikoba ya uenyekiti wa COMESA na mwenyekiti anayeondoka, Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye

Rais William Ruto ndiye mwenyekiti mpya wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA). 

Ruto amekabidhiwa wadhifa huo na mtangulizi wake ambaye ni Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye wakati wa kufungwa kwa Kongamano la 24 la COMESA leo Alhamisi.

Kenya imekuwa mwenyeji wa kongamano hilo lililoandaliwa katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC, jijini Nairobi tangu siku ya Jumatatu wiki hii.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Rais Ruto alitoa wito kwa nchi wanachama wa COMESA kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali, uongozi wa data na uwezeshaji wa rasilimali watu ili kuwawezesha raia wa eneo la mashariki na kusini mwa Afrika kujiendeleza katika uchumi wa kidijitali.

“Utumiaji wa mifumo ya kidijitali utasaidia kuboresha matumizi ya rasilimali, kuboresha manufaa ya nishati, na kuwezesha gridi za kisasa za umeme,” alisema kiongozi wa nchi.

“Pia utasaidia kuboresha biashara ya kuvuka mpaka, kuimarisha usafirishaji, ujumuishaji wa kifedha na kubuni majukwaa mapya yatakayowezesha mashirika madogo na ya kati kufikia masoko ya kikanda na kimataifa.”

Kongamano hilo lilihudhuriwa na Marais Évariste Ndayishimiye wa Burundi, Azali Assoumani (Comoros) na Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe.

Pia lilihudhuriwa na Mawaziri Wakuu Ahmed Abiy wa Ethiopia, Russell Mmiso Dlamini (Eswatini), na Mustafa Madbouly wa Misri.

Wengine waliohudhuria ni mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC)  Mahmoud Youssouf, Katibu Mkuu wa COMESA Chileshe Mpundu Kapwepwe na mwenyekiti wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika, Wamkele Mene.

Website |  + posts
Share This Article