Rais William Ruto amefichua kwamba sehemu ya ukuta wa uzio katika Ikulu ya Nairobi itabomolewa baada ya kugunduliwa kwamba iko kwenye ukingo wa mto.
Alisema haya alipokuwa akihutubia bunge la kaunti ya Nairobi leo Alhamisi Aprili 9, 2026 ambapo alielezea kwamba kundi la maafisa wa idara mbali mbali lililojukumiwa kutambua maeneo ya karibu na mito lilitoa notisi kuhusu ukuta huo.
Kiongozi wa nchi alisisitiza kwamba ukuta huo karibu na mto Kirichwa Kubwa ni lazima ubomolewe kulingana na kanuni za kimazingira na kwamba Ikulu haijasaazwa na sheria.
“Nimepokea notisi kwamba sehemu ya ukuta wa uzio wa Ikulu karibu na maanguko ya maji ya mto Kirichwa Kubwa iko kwenye ukingo wa mto na ni lazima ibomolewe.” Alisema Rais.
Alieleza zaidi kuwa kanuni zinahitaji kuwepo kwa eneo la kinga la angalau mita 15 kutoka alama ya kiwango cha juu cha maji, ikimaanisha kuwa ukuta huo lazima urekebishwe ili kuafikia viwango vya kisheria.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi pana za serikali za kurejesha ardhi za kando ya mito na kushughulikia masuala ya mazingira na mafuriko katika maeneo ya miji, hasa Nairobi.
Rais pia aliangazia changamoto zinazokabili taifa, akibainisha kuwa Wakenya wengi, hasa wakazi wa Nairobi, wanadai mifumo bora kama mifereji iliyoboreshwa na udhibiti wa mafuriko, lakini mara nyingi hawako tayari kuunga mkono hatua ngumu zinazohitajika ili kufanikisha hilo.
Alisisitiza kuwa kushughulikia mafuriko ya mara kwa mara jijini kutahusisha hatua ngumu, ikiwa ni pamoja na kuhamisha watu na kubomoa miundombinu iliyojengwa kwenye ardhi za kando ya mito.
Hatuwezi kudai usafi huku tukilinda utupaji taka haramu. Hatuwezi kudai utaratibu huku tukipinga kila hatua inayohitajika kuufanikisha,” alisema Ruto.