Rais Ruto aanzisha mashindano ya 71 ya Safari Rally

Dismas Otuke
2 Min Read
Rais William Ruto akipiga picha na madereva wanaoshiriki mashindano ya mwaka huu ya WRC Safari rally

Rais William Ruto siku ya Alhamisi alianzisha makala ya 71 ya mashindano ya magari nje ya ukumbi wa KICC ambayo pia ni mkondo wa tatu wa mbio za magari ulimwenguni WRC mwaka huu.

Katika hafla hiyo, bingwa mara tano wa mashindano hayo Carl Tundo alikuwa wa kwanza kuondoka jukwaani akielekezwa na Tim Jessop wakiendesha gari aina ya Skoda Fabia.

Bingwa mtetezi wa bara Afrika Karan Patel alikuwa wa pili kuondoka akisaidiwa na Tauseef Khan wakiendesha gari aina ya Skoda Fabia.

Rais amekariri kujitolea kwa serikali kuendelea kuyaunga mkono mashindano hayo ambayo yanatangaza vyema Kenya kama kituo bora cha utalii na uwekezaji kando na kutoa fursa za kujiendeleza kwa wajasiriamali wa humu nchini.

Baada ya uzinduzi huo, magari yalielekea katika kituo cha Kasarani ambapo madereva walishindana ana kwa ana katika umbali wa kilomita 4.8.

Mashindano hayo yataelekea Naivasha kwa siku tatu zijazo, madereva wakishindana siku ya Ijumaa katika vituo vya Loldia 1, Geothermal 1 na Kedong kabla ya kurudia tena.

Siku ya Jumamosi, madereva watashindana katika vituo vya Soysambu, Elementeita na hatimaye Sleeping Warrior na kurudia tena mchana ili kukamilisha siku ya tatu.

Jumapili, madereva wataanzia Malewa waelekee Oserengoni na hatimaye Hells Gate na kurudia vituo hivyo, ili kuhitimisha makala ya mwaka huu ya mashindano ya Safari Rally.

Madereva watashindana jumla ya umbali wa kilomita 367.67.

Share This Article