Rais William Ruto ametoa hakikisho kwa Wakenya kwamba utawala wake utaendelea kulinda uhuru wa kidini nchini.
Hata hivyo, amesema kuna haja ya kuepusha matumizi mabaya ya dini kuwadhuru raia.
“Tutaendelea kulinda uhuru wa kidini, lakini wakati huohuo kuepusha uwezekano wa matumizi yake mabaya kuwadhuru Wakenya,” amesema Rais Ruto.
Aliyasema hayo wakati alipokabidhiwa ripoti ya Jopokazi la Rais juu ya Mapitio ya Mpangokazi wa Kisheria na Udhibiti Unaoongoza Makundi ya Kidini humu nchini.
Jopokazi hilo liliongozwa na aliyekuwa mbunge wa Mbeere Kusini Mutava Musyimi ambaye pia wakati mmoja alihudumu kama Katibu Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Makanisa nchini, NCCK.
Ripoti hiyo imewasilishwa wakati ambapo kumekuwa na miito ya kudhiti taasisi za kidini nchini kutokana na matumizi yake mabaya kwa lengo la kuwapunja Wakenya.
Aidha, kumekuwa na maafa yaliyotokana na itikadi za kutiliwa shaka kama ilivyokuwa katika eneo la Shakahola ambapo watu kadhaa waliripotiwa kufariki baada ya kufunga kwa siku kadhaa bila kula.