Rais William ruto na Naibu Rais Kithure Kindiki wamemwomboleza mwakilishi wadi mteule wa chama cha UDA katika kaunti ya Nyandarua Beth Wahito.
Kupitia akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii, Rais Ruto aliandika, “Tunaungana na familia na watu wa kaunti ya Nyandarua kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Beth Wahito”.
Kiongozi wa nchi aliendelea kumsifia mwendazake akimtaja kuwa mwanaharakati shupavu wa chama cha UDA mashinani ambaye aliamini katika siasa za maendeleo.
“Beth atakumbukwa kwa mawazo mengi mapya ambayo yamebadilisha maisha ya watu wa Njabini. Lala salama Mheshimiwa Beth” alimalizia Rais Ruto.
Naibu Rais Kithure Kindiki naye alisema amehuzunishwa na taarifa za kifo cha kusikitisha cha Beth Wahito, ambaye atakumbukwa kwa kujitolea kwake kwa uwezeshaji kiuchumi wa watu wa Njabini.
“Pole kwa familia, viongozi wenzake, marafiki na wakazi wa kaunti ya Nyandarua” aliandika Kindiki.
Mheshimiwa Beth Wahito, alifariki Jumamosi usiku katika ajali kwenye barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea Nakuru alipokuwa akitoka kwenye mkutano wa kamati ya bajeti ya bunge la kaunti ya Nyandarua.
Spika wa kaunti ya Nyandarua Stephen Wachira Waiganjo alielezea kwamba Beth aligongwa na basi la kampuni ya Guardian alipokuwa akijaribu kuvuka barabara na akafariki papo hapo.
Wahito ni mwanasiasa mzoefu ambaye amekuwa katika ulingo wa siasa kwa zaidi ya miongo mitatu.