Rais Museveni aipongeza Uganda Cranes kwa kufuzu AFCON

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameilimbikizia sifa sufufu timu ya taifa ya nchi hiyo ya Uganda Cranes kwa kufuzu fainali za 35 za kipute cha mataifa ya bara la Afrika, AFCON. 

Kipute hicho, kinachosakatwa kila baada ya miaka miwili, kitaandaliwa mwakani nchini Morocco.

Hii ni mara ya tatu kwa Uganda Cranes kufuzu mashindano hayo katika kipindi cha miaka minane iliyopita.

“Naipongeza Uganda Cranes kwa kufuzu mashindano ya AFCON,” alisema Rais Museveni katika taarifa ya kusherehekea ushindi wa timu hiyo.

“Nawapongeza wachezaji, makocha, FUFA, Wizara ya Elimu na Michezo, na Waganda wenzangu wote.”

Rais Museveni amehusisha ushindi huo na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali yake kuboresha miundombinu ya michezo nchini humo na ameahidi kuwa uwekezaji zaidi utaendelea kufanywa.

Taifa Stars ya Tanzania ni timu nyingine ambayo imejikatia tiketi ya kushirik mashindano hayo.

Hii ni baada ya timu hiyo kuwanyofoa tembo wa Guinea bao moja bila jawabu katika mchuano wa mwisho wa kufuzu wa kundi H jana Jumanne alasiri ugani Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Taifa Stars walifuzu kwa AFCON mara ya kwanza mwaka 1980, kabla ya kurejea tena mwaka 2019 nchini Misri na mwaka huu kwa mara ya tatu.

Tanzania wanajiunga na waandalizi wenza wa fainali za AFCON mwaka 2027, Uganda Cranes, ambao wamefuzu huku Kenya ikiwa mwenyeji mwenza pekee kufungiwa nje ya safari ya Morocco mwaka ujao.

Morocco itaandaa kipute cha AFCON cha makala ya 35 kati ya Disemba 21 mwaka ujao na Januari 18 mwaka 2026.

 

Share This Article