Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ametoa wito wa kudumishwa kwa amani, huku akiwataka viongozi kukumbatia mazungumzo.
Kupitia kwa taarifa kwa vyombo vya habari Jumanne usiku, Rais huyo wa zamani, aliwakumbusha viongozi kuwa ni wajibu wao kuwasikiliza wananchi waliowachagua jinsi ilivyoratibiwa kwa katiba.
“Kuwasikiliza wananchi sio chaguo, mbali ni jukumu la kikatiba na ni demokrasia,” alisema Uhuru.
“Wakati huu ningependa kuwakumbusha viongozi kwamba, walichaguliwa na wananchi,” aliongeza Rais huyo mstaafu.
Huku akiwaomboleza waandamanaji waliopoteza maisha walipokuwa wakishiriki maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024, Uhuru alisema serikali haipaswi kutumia nguvu dhidi ya wakenya wanaotekeleza haki yao ya kikatiba.
“Ghasia sio jawabu. Kama Rais wenu mstaafu, naelewa uzito uliopo katika kuongoza Kenya, na hivyo naomba hekima na ustaarabu na amani na ustawi ziwe kwetu sote kama watoto wa taifa hili,” alisema Uhuru.
Uhuru vile vile alitoa wito kwa serikali ya sasa kushiriki meza ya mazungumzo na wananchi.
“Naomba kuwe na maelewano baina ya kila mkenya na kila mmoja wetu afahamu kuwa Kenya ni kubwa kutuliko sisi,” alidokeza Uhuru Kenyatta.