Rais wa Marekani anayeondoka madarakani Joe Biden ametangaza msamaha kwa mwanawe Hunter ambaye alistahili kuhukumiwa mwezi huu kwenye kesi ya uhalifu.
Hunter alikubali mashtaka ya matumizi mabaya ya silaha aina ya bunduki na mengine yanayohusiana na ushuru mwezi Septemba.
Alipatikana na hatia ya kutumia dawa kinyume cha sheria na kumiliki bunduki na hivyo kuwa mwana wa kwanza wa Rais aliye madarakani kupatikana na hatia.
Rais huyo wa chama cha Democratic alikuwa amesema awali kwamba hangemsamehe mwanawe au kumpunguzia adhabu.
Lakini jana Jumapili akitangaza msamaha huo, Rais Biden alisema kwamba hata ingawa anaamini katika mfumo wa haki wa Marekani, siasa zimeingilia mchakato mzima na kuhujumu haki.
Rais mteule wa Marekani Donald Trump ametaja msamaha huo kuwa matumizi mabaya ya mamlaka na hatua ya kuhujumu haki.
Katika kutoa msamaha huo kamili na usio na masharti, Rais Joe Biden alisema Hunter alishtakiwa kwa njia isiyofaa na isiyo ya haki.
Kulingana na Biden, kumekuwa na juhudi za kumvunja Hunter ambaye anasema amekaa kwa miaka mitano unusu bila kutumia dawa za kulevya.
“Katika kujaribu kumvunja Hunter, wamejaribu kunivunja pia na hakuna sababu ya kuamini kwamba juhudi zao zitakomea hapa.” alisema Rais Biden katika taarifa.
Msamaha huo ni kwa makosa yote anayodaiwa kutekeleza Hunter kutoka Januari 2014 hadi Disemba 2024.
Kipindi hicho kinahusisha muda ambao Biden alihudumu kwenye bodi ya kampuni ya Burisama, ya Ukraine ambayo inadaiwa kutekeleza makosa ya kutoa hongo.