Rais Biden ahojiwa kuhusu nyaraka za siri

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais wa Marekani Joe Biden.

Rais Joe Biden wa Marekani amehojiwa ikiwa ni sehemu ya uchunguzi huru kuhusu jinsi alivyoshughulikia nyaraka za siri, Ikulu ya Marekani imesema.

Msemaji wa ikulu hiyo Ian Sams alisema katika taarifa kwamba mahojiano hayo yalikuwa ya hiari na yalifanyika katika Ikulu ya Marekani siku za Jumapili na Jumatatu.

Mahojiano hayo yalihitimishwa Jumatatu.

Uchunguzi huo unaongozwa na wakili maalum Robert Hur, ambaye aliteuliwa na Mwanasheria Mkuu Merrick Garland kusimamia suala hilo nyeti kisiasa ili kuepusha migongano ya kimaslahi.

Sams alisisitiza kwamba Rais Biden na Ikulu ya Marekani wanashirikiana. Alielekeza maswali kwa Wizara ya Sheria.

Nyaraka za kwanza zilipatikana Novemba 2, 2022 katika kituo cha Penn Biden kilichoanzishwa na Rais huyo jijini  Washington DC.

Nyaraka zingine zilipatikana Disemba 20 katika eneo la kuegesha gari nyumbani kwake  Wilmington, huku zingine zikipatikana Januari 12 mwaka huu, walisema mawakili wake.

Haikufahamika ni kwa nini Rais Biden aliweka nyaraka hizo za siri.

TAGGED:
Share This Article