Rais William Ruto ameagiza wizara ya kawi iwafute kazi maafisa wote wa serikali wanaodaiwa kutoa leseni ya kuidhinisha kinyume cha sheria shughuli za kiwanda cha Gesi ambapo mkasa wa moto ulitokea siku ya Alhamisi Mtaani Embakasi, jijini Nairobi.
Akiongea katika eneo bunge la Lugari Kaunti ya Kakamega Jumamosi asubuhi, Rais Ruto alisema tukio hilo linatokana na ufisadi, ukosefu wa uadilifu na tamaa miongoni mwa maafisa wa serikali.
Ruto alielezea wasiwasi kwamba maafisa fulani serikalini walikuwa wameiidhinisha biashara hiyo kuendeshwa kwenye makazi ya watu, hali inayohatarisha maisha yao.
“Kuna watu wenye leseni katika maeneo ya makazi na wanahatarisha maisha ya raia. Nimeagiza wizara husika kwamba wale wote waliohusika na utoaji wa leseni mahali ambapo haikustahili wafutwe kazi na kupelekwa mahakani. Hawa watu wanajua kuwa waliambiwa hawatapewa leseni lakini kwasababu ya ufisadi na kukosa uaminifu, walipewa leseni na kuendelea na shughuli zao,’’
Watu watatu waliaga dunia na takriban wengine 280 kujeruhiwa kwenye mkasa huo, katika eneo la Mradi baada ya mtambo wa kujaza na kuhifadhia gesi kushika moto.