Kiongozi wa muungano wa upinzani Raila Odinga leo ametoa taarifa kuhusu ripoti ya kamati ya pamoja ya mazungumzo ya maridhiano.
Katika hotuba kwa wanahabari Raila alisema kwamba ripoti hiyo ni hatua nzuri ya mwanzo japo haijakamilika.
Wabunge wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya waliidhinisha ripoti hiyo katika mkutano wao ulioandaliwa kabla ya kikao na wanahabari.
Kulingana na Raila, wawakilishi wa muungano huo katika kamati ya mazungumzo ya maridhiano waliafikia baadhi ya malengo yao kama mabadiliko katika tume ya uchaguzi nchini IEBC na nyongeza ya mgao wa fedha kwa serikali za kaunti.
Kuhusu uundaji wa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani na afisi ya waziri mkuu, Raila alipendekeza maamuzi yafanywe na wakenya kupitia kura ya maamuzi.
Kamati hiyo ya mazungumzo ya maridhiano ilikuwa chini ya uongozi wa Kalonzo Musyoka na Kimani Ichung’wa.
Ilikamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti ya mwisho kwa viongozi husika Jumamosi, Novemba 25, 2023 kwa njia ya kielektroniki.