Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga ameendeleza kampeni yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC mjini New York nchini Marekani, pembezoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Raila anahudhuria kikao hicho akiandamana na Rais William Ruto.
Jana Jumatatu, alikutana na Rais wa Senegal Diomaye Faye kutafuta uungwaji mkono kwenye azima yake.
Ruto na Raila pia wamepanga mikutano na Marais na wawakilishi wa mataifa ya Afrika wanaohudhuria kikao hicho.
Tayari Raila amepata uungwaji mkono kutoka kwa mataifa ya Afrika Mashariki na mataifa mengine yanayozungumza Kiingereza.
Mpinzani mkuu wa Raila katika kinyang’anyiro hicho cha Februari mwaka ujao ni Mahamoud Ali Youssouf, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti.
Bara Afrika linajumuisha mataifa 23 yanayozungumza Kiingereza na mengine 21 yanayozungumza Kifaransa, 6 yanazungumza Kireno na 13 yanatumia Kiarabu kama lugha rasmi.
Kulingana na Umoja wa Afrika, mwaka ujao utakuwa zamu ya Afrika Mashariki kutwaa uenyekiti wa tume hiyo.