Mwaniaji wa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) Raila Odinga, amesema lengo lake kuu ni kuunganisha bara hili, akisema kuwa atashirikiana na marais wote wa Afrika kutimiza lengo hilo.
Akizungumza leo wakati wa sherehe ya kumzindua rasmi kuwania wadhifa huo iliyoandaliwa katika ikulu ya Nairobi, Raila alielezea haja ya bara hili kuungana ili kupiga hatua na kutimiza ndoto za waanzilishi wa mataifa ya bara hili.
“Ni lazima bara Afrika liungane la sivyo litaangamia. Ili kutimiza ndoto za waanzilishi wa bara hili, lazima kwanza kuwe na amani barani humu,” alisema Raila.
Raila alisema yuko tayari kuwahudumia raia wa bara hili kwa uadilifu na kufanikisha maendeleo barani humu.
“Niko tayari kuhudumu, roho yangu iko tayari na mikono yangu iko tayari, na kupitia usaidizi wenu nitapata fursa ya kuhudumia bara hili,” alisema Raila.
Baadhi ya Marais waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Rais wa Tanzania Samia Suluhu, Yoweri Museveni wa Uganda, Salva Kiir wa Sudan Kusini na waziri mkuu wa Burundi Gervais Ndirakobuca.
Marais wa zamani Jakaya Kikwete wa Tanzania na Olusegun Obasanjo wa Nigeria, pia walihudhuria.