Raila kwenye ziara ya kibinafsi Uingereza

Marion Bosire
2 Min Read
Kiongozi wa Upinzani Raila odinga.

Kiongozi wa muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga yuko kwenye ziara nchini Uingereza. Kwenye taarifa afisi yake ilitaja ziara hiyo kuwa ya kibinafsi na kibiashara.

Msemaji wa Raila kwa jina Denis Onyango alisema waziri huyo mkuu wa zamani pia atatumia ziara hiyo kwa mapumziko.

Akiwa nchini Uingereza, Onyango alisema Raila atakutana na marafiki,jamaa na washirika wa kibiashara.Anatarajiwa kurejea nchini mwishoni mwa juma.

Ziara yake ilijiri muda mfupi baada yake kumkanya vikali balozi wa Marekani humu nchini Meg Whitman kuhusiana na uchaguzi mkuu uliopita.

Whitman kwenye kongamano la 8 la ugatuzi mjini Eldoret alisema kwamba uchaguzi mkuu uliopita uliendeshwa kwa njia wazi na ulikuwa wa haki.

Raila kwenye kongamano hilo hilo lakini siku tofauti alimwambia balozi huyo akome kuzungumzia masuala ya Kenya. Hii inatokana na ukweli kwamba upande wa upinzani unaamini kwamba uchaguzi wa urais kwenye uchaguzi mkuu uliopita haukuwa wa haki ingawaje mahakama ya upeo ilihalalisha ushindi wa Rais William Ruto.

Akiwa katika uwanja wa ndege kabla ya kuondoka kuelekea Uingereza, Raila alikutana tena na Seneta wa Marekani Chris Coons ambaye pia alikuwa anaabiri ndege kurejea nyumbani.

Seneta Coons amekuwa nchini Kenya ambapo aliandaa mazungumzo kwanza na Raila Odinga na baadaye akashauriana na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Inakisiwa kwamba ziara ya Coons ni ya kutafuta maridhiano kati ya Raila na Rais Ruto.

Website |  + posts
Share This Article