Raila kukabiliana na wagombeaji watatu kuwania uenyekiti wa AUC

Tom Mathinji
1 Min Read
Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Wawaniaji wawili zaidi wamejiunga kwenye kinyang’anyiro cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika,AUC,  huku shughuli ya kuwasilisha stakabadhi za uteuzi ikikamilika Jumanne.

Wawaniaji wa hivi punde kujitosa ulingoni ni kutoka mataifa ya Madagascar na Mauritius ambao sasa watakabana koo na aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf.

Umoja wa Afrika ulitenga Jumanne tarehe 6, kuwa siku ya mwisho ya kuwasilishwa stakabadhi za uteuzi kwa wanaonuia kuwania kiti hicho na nafasi za makamishna.

Wawaniaji hao wanne wanalenga kuchukua nafasi ya mwenyekiti anayeondoka Moussa Faki Mahamat, aliyehudumu kwa mihula miwili.

Kwenye taarifa Jumatatu tume hiyo ilisema ni majina tu ya wawaniaji yatakayowasilishwa na kanda ndio yatakubaliwa kushiriki uchaguzi.

Aidha tume hiyo ilisema ni wawaniaji kutoka mataifa ambayo hayajawekewa vikwazo vyovyote na Umoja wa Afrika ndio watakubaliwa kushiriki uchaguzi utakaoandaliwa mwezi Februari mwakani.

Share This Article