Kiongozi wa upinzani Raila Odinga sasa anataka kila familia iliyoathiriwa na mlipuko wa gesi uliotokea katika eneo la Embakasi, kaunti ya Nairobi ilipwe fidia ya shilingi 500,000 pesa taslimu.
Angalau watu sita wamethibitishwa kufariki kutokana na mkasa huo uliotokea wiki jana huku mamia ya wengine wakiendelea kupokea matibabu katika hospitali mbalimbali.
Raila ameilaumu serikali akidai utepetevu wake ulichangia kutokea kwa mkasa huo.
“Kila familia iliyoathiriwa na moto uliotokea wiki jana uliosababishwa na mlipuko wa gesi katika eneo la Embakasi inapaswa kulipwa fidia ya shilingi 500,000. Huu ni utepetevu uliotokea kwa upande wa utawala wa Kenya Kwanza,” alisema Raila alipotembelea baadhi ya waathiriwa wa mkasa huo akiandamana na mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.
Aliyasema hayo huku washukiwa wanne wanaohusishwa na mlipuko wa gesi uliotokea katika eneo la Embakasi wakifikishwa katika mahakama moja ya Milimani leo Jumanne.
Wanne hao wanajumuisha Derrick Kimathi ambaye ni mmiliki wa kituo hicho cha kuuza gesi pamoja na David Ongare, Joseph Makau na Marrian Kioko ambao ni maafisa wa halmashauri ya usimamizi wa mazingira, NEMA.
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama iwazuilie washukiwa hao ili kuwapa maafisa wa polisi muda wa kukamilisha uchunguzi. Kimathi alizuiliwa katika kituo cha polisi cha Embakasi baada ya kujisalimisha jana Jumatatu.
Idara ya DCI imesema bado inawatafuta washukiwa wengine watano.
Washukiwa hao ni pamoja na Stephen Kilonzo ambaye ni msimamizi wa eneo la kituo hicho, Ann Kabiri Mirungi na Lynette Cheruiyot wa NEMA, dereva wa lori Robert Gitau na dereva mwingine aliyetambuliwa kama Abraham Mwangi.
Kisa hicho cha Alhamisi wiki iliyopita kilitokea baada ya lori lililokuwa limebeba mitungi ya gesi kulipuka mwendo wa saa tano unusu usiku na kusababisha moto mkubwa.