Raila azuiwa kuingia eneo ambako ubomozi unaendelea Mavoko

Marion Bosire
2 Min Read

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amezuiwa kuingia katika eneo ambako ubomozi wa nyumba unaendelea katika ardhi ya kampuni ya saruji ya East African Cement Portland, EAPC huko Mavoko katika kaunti ya Machakos.

Raila ambaye alifika katika eneo hilo kujionea yanayoendelea alikatazwa kuingia katika eneo hilo na maafisa wa polisi ambao walisema iwapo angeingia katika eneo hilo, angekatiza kazi ambayo inaendelea.

Alikuwa ameandamana na viongozi wengine akiwemo kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti, Maseneta Stewart Madzayo wa Kilifi na Edwin Sifuna wa Nairobi kati ya wengine alipozuiwa kufika katika eneo hilo.

Kiongozi huyo alilazimika kuhutubia wanahabari barabarani ambapo alilaani ubomozi huo wa makazi ya watu akisema Rais alikuwa amekwenda kinyume cha ahadi yake wakati wa kampeni ya kuhakikisha kwamba ufurushaji wa watu ungesitishwa.

Alisema kulingana na ahadi ya Rais, waathiriwa wa jambo kama hilo wangesaidiwa na serikali kupata makao mbadala kabla ya nyumba zao kubomolewa lakini hilo halikufanyika.

Alishangaa kwamba mashirika ya kutetea haki za binadamu hayajasema lolote wakati ambapo ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unatekelezwa, kupitia ubomoaji wa nyumba ambazo wengine walijenga kwa kutumia akiba zao za maisha.

Wakenya wengi wanakadiria hasara ya mamilioni ya pesa baada ya nyumba zao kubomolewa katika ardhi hiyo ya EAPC siku chache baada ya mahakama kuamua kwamba kampuni hiyo hiyo ndiyo mmiliki wa ardhi hiyo.

Raila sasa anasema wamejitolea kama chama cha Azimio la Umoja One Kenya kuhakikisha kwamba wahasiriwa wa ubomozi huo wamefidiwa.

Share This Article