Raila atoa wito wa kutolewa kwa fedha zilizotengewa ugatuzi

Tom Mathinji
2 Min Read
Kiongozi wa upinzani Raila odinga.

Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, ametoa wito wa kutolewa kwa fedha zilizotengewa majukumu yaliyogatuliwa kwa serikali za kaunti.

Raila alilalamika kwa kile alichokitaja kuwa na majukumu yanayofanana katika serikali ya kitaifa na zile za kaunti, miaka 10 baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi hapa nchini.

“Fedha nyingi zinaendelea kutumika katika wizara ya afya, ile ya kilimo na wizara ya maji, katika majukumu ambayo tayari yamegatuliwa. katika sheria ya fedha ya mwaka 2023, bajeti ya afya imeongezeka kwa shilingi bilioni 32 katika kiwango cha kitaifa, ikizingatiwa kuwa majukumu ya afya yamegatuliwa,”alisema Raila.

Akizungumza katika kongamano linaloendelea kuhusu ugatuzi katika kaunti ya Uasin Gishu, kiongozi huyo wa upinzani aliitaka serikali ya kitaifa kuzingatia kikamilifu sheria, na kuruhusu serikali za kaunti kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa katiba.

“Hii leo mbolea ya bei nafuu inanunuliwa na kusambazwa na serikali ku. nyumba za gharama nafuu zinajengwa na serikali ya kitaifa. Serikali inalenga kujenga masoko na kuwaajiri wahudumu wa afya wa kijamii. majukumu hayo yote yamegatuliwa ambapo fedha zilizotengewa majukumu hayo zinapaswa kutolewa kwa serikali za kaunti,”alidokeza Raila.

Aidha Kiongozi  huyo wa  Azimio, alipongeza baraza la magavana kwa kujiepusha na siasa za uhasama na migawanyiko.

Raila alisema  katika  miaka kumi ya ugatuzi, nchi hii imeshuhudia ufufuo na mabadiliko ya kiuchumi katika maeneo ya mashambani.

Website |  + posts
Share This Article