Raila azungumzia mkutano kati ya Ruto na Jaji Mkuu Koome

Marion Bosire
2 Min Read

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ametoa maoni yake kuhusu tangazo la Jaji Mkuu Martha Koome kwamba wameomba kukutana na Rais William Ruto.

Ombi la jaji mkuu linafuatia shutuma za viongozi kutoka asasi mbili za serikali dhidi ya idara ya mahakama kwamba idara hiyo ina maafisa wafisadi wanaolemaza mipango ya serikali.

Raila anahisi kwamba Koome na wenzake wakifanya mkutano na Rais Ruto watahujumu mahakama ikitizamiwa kwamba kuna kesi dhidi ya serikali kuu kortini na ambayo uamuzi wake unafaa kutolewa Januari 25, 2024.

Alikuwa akizungumza huko Vihiga ambapo alisema mkutano huo haufai na kwamba sheria inatoa fursa ya kukata rufaa kwa yeyote asiyeridhika na maamuzi ya mahakama.

Kiongozi huyo wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya anasema Koome tayari ametangaza msimamo kuhusu madai ya uwepo wa maafisa wafisadi katika idara yake na hilo linatosha.

Jana Jumatatu jaji mkuu Martha Koome alisema kwamba idara ya mahakama imemwandikia Rais waraka wa kuomba mkutano naye ili kujadili kuhusu usemi wake.

Rais Ruto kwa upande wake amesema kwamba yuko tayari kukutanga na uongozi wa idara hiyo ya mahakama ili kuondoa ufisadi ambao anasema unakwamisha mipango ya maendeleo ya serikali.

Mahakama zilisimamisha utekelezaji wa sheria ya fedha ya mwaka 2023 na utekelezaji wa mpango mpya wa bima ya afya.

Share This Article