Aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ametetea operesheni za kampuni ya Adani Group, akisema tajiriba ya kampuni hiyo ni ya kupigiwa mfano.
Kulingana na Raila, hali ya kampuni hiyo imeelezewa visivyo, hasaa baada ya kutia saini mkataba wa maelewano na serikali kuwekeza katika usimamizi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na katika sekta ya nishati nchini.
“Kumekuwa na habari ambazo si za kweli kuhusu Adani. Kulingana na ufahamui wangu kampuni hii ina tajiriba ya kupigwa mfano. Kampuni hii imetekeleza miradi mingi kati ya serikali na sekta za kibinafsi,” alisema Raila.
Mgombea huyo wa Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika anasema kuwa hali ya kiuchumi nchini ambapo kodi haiwezi kukidhi mahitaji ya maendeleo,taifa hili linahitaji mikataba hiyo kwa ukuaji wa miundombinu.
Raila alisema kuwa sheria za ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi nchini Kenya- PPP zinatokana na zile za India na Gujarat, ambako Adani amekuwa na jukumu kubwa katika maendeleo ya miundombinu.
Hata hivyo, alitahadharisha kuwa mfumo uliopo ni sharti uboreshwe ili kuvutia na kuleta imani ya wawekezaji.
Raila alisema kumekuwa na hofu kuhusu jinsi mchakato wa PPP wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta-JKIA na sekta ya nishati ulivyoshughulikiwa.
Hata hivyo ameitaka serikali kushughulikia maswala ya umma yaliyotolewa kwa uwazi, kuhakikisha kuwa mchakato huo umewekwa wazi,na kutoa fursa ya ushindani kwa njia ya haki.