Kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga sasa anataka sheria ya fedha ya mwaka wa 2023 ifutiliwe mbali.
Raila, aliyewasili nchini siku ya Jumanne, alisema atatumia kila mbinu ikiwa ni pamoja na kufanya maandamano kuhakikisha sheria hiyo inaondolewa.
“Hakuna njia mbadala iliyosalia, lazima tupigane, tutapigana kila mahali hadi pale sheria hiyo itakapofutiliwa mbali,” alisKma wakati akiwahutubia wafuasi wake katika uwanja wa kamukunji.
Alilaumu serikali na wabunge kwa kuwahadaa Wakenya wakati huu mgumu kupitia hatua aliyosema itasababisha kupanda zaidi kwa gharama ya maisha nchini.
Aliyasema hayo siku moja baada ya Rais William Ruto kuutia saini kuwa sheria mswada wa fedha wa mwaka 2023 katika Ikulu ya Nairobi.
Muungano wa Azimio umepinga vikali hatua ya serikali ya Kenya Kwanza kuongeza ushuru ziada wa thamani kwa bidhaa za mafuta kutoka asilimia nane hadi asilimia 16, ukisema hatua hiyo itawaongezea Wakenya mzigo.