Raila abwagwa katika uchaguzi wa AUC

Dismas Otuke
1 Min Read

Mwaniaji wa Kenya wa kiti cha tume ya Umoja wa Afrika – AUC, Raila Odinga, ameshindwa kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti.

Raila alizimika kujiondoa katika raundi ya sita baada ya kupata kura 21 dhidi ya 26 za Mohamoud Ali Yousouf wa Djibouti.

Kura hizo ziliingia raundi sita baada ya mshindi kukosekana katika raundi tatu za kwanza, na kumlazimu Richard  Ramandrianto wa Madagascar kujiondoa.

Kenya ilipata kura 20 katika raundi ya kwanza dhidi ya 18 za Djibouti, huku Madagascar ikizoa kura 10.

Kwenye raundi ya pili, Kenya ilipata kura 22 dhidi ya 19 za Djibouti, wakati Madagascar ikijipatia kura 7.

Mambo yaligeuka katika raundi ya tatu, Kenya ikipata kura 21, dhidi ya Djibouti iliyopata 25, nayo Madagascar ikajipatia kura 5.

Raundi ya nne ilishuhudia Djibouti ikipata kura 25, huku Kenya ikijipatia 21, kura moja ikaharibika na mataifa mawili yakakosa kushiriki.

Raundi ya tano, Kenya ilisalia na kura 21, Djibouti 26, ikisalia hivyo katika raundi ya sita na kumlazimu Raila kujiondoa.

Yousouf amepata ushindi katika raundi ya saba baada ya kupata kura 33, na ndiye mwenyekiti mpya wa AUC, akimrithi Mousa Faki wa Chad.

Share This Article