Raila ashauriana na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir

Tom Mathinji
2 Min Read
Raila Odinga ashiriki mazungumzo na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.

Mjumbe maalum wa Kenya nchini Sudan Kusini Raila Odinga, ameshiriki mazungumzo na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kuhusu mzozo wa kisiasa unaoghubika taifa hilo.

Mazungumzo hayo ya viongozi hao wawili, yaliandaliwa Ijumaa katika mji mkuu Juba, lengo kuu likiwa ni kuleta amani na usalama nchini humo na kanda hii kwa jumla.

“Nilikuwa na mazungumzo mazuri na yenye kuzaa matunda na ndugu yangu Rais Salva Kiir, kuhusu hali ya kisiasa nchini humo,” alisema Raila kupitia ukurasa wa X.

Raila alielezea matumaini kwamba mazungumzo hayo yaliashiria uwezekano wa kupatikana suluhu kwa mzozo unaoghubika Sudan Kusini, akidokeza kuwa atawafahamisha viongozi wengine wa kanda hii akiwemo Rais William ruto, kuhusu matokeo ya mkutano huo.

Waziri huyo Mkuu wa zamani wa Kenya alisafiri kuelekea Sudan Kusini siku ya Ijumaa, baada ya kuteuliwa na Rais William Ruto kuwa mjumbe wake Sudan Kusini, ili kusuluhisha mzozo wa kisiasa kufuatia kukamatwa na kuzuiliwa kwa Makamu wa kwanza wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar

Raila Odinga atua Uganda kwa mazungumzo na Rais Yoweri Museveni.

Baadaye Raila alisafiri hadi nchini Uganda, na kukutana na Rais Yoweri Museveni, ambapo alimfahamisha kuhusu mazungumzo yake na Rais Kiir.

“Nimewasili Jijini Entebe, Uganda kumfahamisha Rais Yoweri Museveni kuhusu ziara yangu nchini Sudan Kusini na hali ya kisiasa nchini humo. Nina matumaini kwamba amani itapatikana Sudan Kusini,’ alisema Odinga.

Hali ya wasiwasi ilizidi kutanda nchini Sudan Kusini baada ya Makamu wa kwanza wa Rais wa taifa hilo Riek Machar kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani.

Jamii ya kimataifa inaendelea kutoa wito wa kuachiliwa huru kwa Riek Machar, huku Rais Kiir na Machar wakitakiwa kushiriki meza ya mazungumzo na kusitisha ghasia nchini humo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *