Mabalozi kutoka nchi mbalimbali za bara la Afrika wametakiwa kuunga mkono juhudi za kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.
Akiwarai kumuunga mkono, Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi aliwakumbusha kuwa ni wakati wa Afrika Mashariki kushikilia wadhifa huo.
“Ikizingatiwa ni wakati wa Afrika Mashariki kushikilia wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC, nilitoa wito kwa mabalozi hao kuunga mkono juhudi za Kenya,” alisema Mudavadi.
Aliyasema hayo baada ya kukutana na kundi la mabalozi kutoka Afrika waliotumwa kuhudumu Nairobi.
Wakati wa mkutano huo, Mudavadi alielezea kujitolea kwa Kenya kutekeleza Ajenda ya Afrika kupitia vipaumbele vya sera ya kigeni.
Raila ametangaza nia ya kumrithi Moussa Faki Mahamat kutoka Chad ambaye muda wake wa kuhudumu kama mwenyekiti wa AUC unakaribia kumalizika.