Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ameendelea na kampeni zake za kutafuta uungwaji mkono wa juhudi zake za kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.
Uchaguzi wa wadhifa huo ambao kwa sasa unashikiliwa na Moussa Faki kutoka Chad umepangwa kufanywa mwezi ujao.
Katika azima yake ya kutaka kumrithi Faki, Raila ameitembelea nchi ya Mauritius na kukutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Dkt. Navinchandra Ramgoolam.
Kwenye taarifa, Raila amesema Ramgoolam ameahidi kumuunga mkono kuchukua usukani kama mwenyekiti mpya wa AUC.
Raila amekuwa akitembelea nchi mbalimbali za bara la Afrika kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa bara hilo watakaopiga kura mwezi ujao kumchagua mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika.
Raila anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf ambaye pia anapigiwa upatu kushinda wadhifa huo.
Mwingine aliye kwenye kinyang’anyiro ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar Richard Randriamandrato.