Kiongozi wa upinzani Raila Odinga siku ya Jumatatu alipeleka kampeni zake nchini Morocco katika juhudi za kutafuta uungwaji mkono wa kuwa mwenyeketiki wa Tume ya Umoja wa Afrika – AUC.
Katika ziara yake, Raila alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Nasser Bourita jijini Rabat.
Raila alielezea bayana ajenda yake endapo atapewa fursa hiyo, akisisitiza kuwa analenga kuimarisha utendakazi wa AUC.
Aliongeza kuwa anapanga kuanzisha juhudi za kuyashinikiza mataifa ya Afrika kuondoa viza baina ya raia wake ili kuimarisha biashara na utangamano katika hatua anayosema itahuisha uchumi.
Baadaye, Raila na Bourita waliwahutubia wanahabari huku Bourita akimshukuru Raila kwa ziara hiyo.
Uchaguzi wa AUC umeratibiwa kuandaliwa mwezi Februari mwakani huku Raila akilenga kuwa Mkenya wa kwanza kutwaa wadhifa huo endapo atachaguliwa.