Kiongozi wa upinzani Raila Amolo Odinga amemzuru askofu mkuu mstaafu Zacchaeus Okoth hospitalini.
Kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Raila alichapisha picha akiwa na Askofu Okoth hospitalini huku akimtakia kila la kheri na uponyaji wa haraka.
Alikumbuka pia jukumu lake kuu katika kufanikisha mapito yake hadi nchi Uganda miaka kadhaa iliyopita na akaenda mafichoni kufuatia kile alichokitaja kuwa nyakati ngumu kisiasa humu nchini.
Raila anasema kwamba anasalia kuwa mwingi wa shukrani kwa mazuri aliyotendewa na askofu Okoth.
Okoth alitawazwa kuwa padri mwaka 1968, akateuliwa kuwa askofu wa dayosisi ya Kisumu mwaka 1978 na akawa askofu mkuu wakati jimbo la Kisumu la kanisa katoliki lilifanywa kuwa jimbo kuu mwaka 1990.
Okoth alijihusisha na siasa wazi wazi akiwa askofu mkuu wa Kisumu na anakumbukwa kwa maoni yake kwamba kupitishwa kwa katiba mpya mwaka 2010 hakungesaidia kumaliza tabia ya kutojali sheria nchini kati ya viongozi wa kisiasa.
Wakati huo huo Raila anashikilia kwamba sheria inakubalia wakenya kuandamana kwa njia ya amani wakipatiwa ulinzi na maafisa wa polisi na hivyo hawafau kuumizwa kwa vyovyote na polisi.
Alikuwa akizungumza huko Sega kaunti ya Siaya wakati wa mazishi ya mchekeshaji Fred Omondi aliyeaga dunia kupitia ajali ya barabarani.