Raila amezea mate uenyekiti wa AU

Martin Mwanje
1 Min Read

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesema yuko tayari kuwania wadhifa wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AU. 

Wadhifa huo kwa sasa unashikiliwa na Moussa Faki kutoka Chad ambaye muhula wake wa kuhudumu utakamilika mwezi Februari mwaka ujao.

Akitangaza nia ya kuwania wadhifa huo leo Alhamisi, Raila alisema alipata kuzuru mataifa mengi ya Afrika alipohudumu kama Mwakilishi Mkuu wa Maendeleo ya Miundombinu wa AU.

Anasema wakati za ziara hizo, alipata kufahamu changamoto zinazokabili mataifa mengi ya bara la Afrika na kinachopaswa kufanywa kukabiliana nazo na kuhuisha ukuaji uchumi wa Afrika.

“Kama mtu anayeamini katika umoja wa Afrika, naamini kwamba Afrika inacheza katika ligi ambayo haipaswi kucheza. Nimekuwa nikifanya mashauriano ya kina. Nafikiria niko tayari kulihudumia bara la Afrika. Afrika inastahili mambo bora zaidi,” alisema Raila wakati akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi.

Alikuwa ameandamana na Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo.

“Sina shaka kwamba rafiki yangu Raila Odinga ndiye mtu anayestahili kuchukuwa uongozi wa wadhifa huu. Ikiwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC itamuunga mkono, naamini bara lote litamuunga mkono,” alisema Obasanjo.

 

 

 

Share This Article