Kwa mara nyingine, kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya na chama cha ODM Raila Odinga ameitaka serikali kukoma kulaumu idara ya mahakama kila mara maamuzi yanapokwenda kinyume cha matakwa yake.
Raila alikuwa akizungumza katika kaunti ndogo ya Rongo, kaunti ya Migori kwenye hafla ya mazishi ya mwenyekiti wa chama cha ODM katika kaunti ya Migori, Philip Makabing’o.
Alisema ni kinyume cha sheria kwa Rais Ruto kuendelea kulaumu idara ya mahakama kila inaposimamisha utekelezaji wa sera zinazopendelea serikali.
Rais Ruto amekuwa akisema kwamba ufisadi katika idara ya mahakama unaongoza jinsi majaji wanatoa maamuzi kwenye kesi za kupinga mipango ya serikali kama ada ya nyumba za gharama nafuu na bima ya matibabu.
Raila alimsifia marehemu Mhandisi Philip Makabong’o akisema kujitolea kwake kwa chama cha ODM na mengi mazuri aliyoafikia vitakumbukwa milele.