Kiongozi wa muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga anataka wahasiriwa wote wa ukatili wa polisi wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024 wafidiwe.
Katika ujumbe alioweka kwenye akaunti yake ya mtandao wa X, Raila alisema kwamba polisi hawafai kutumwa kwenye barabara za humu nchini ilhali hakuna hali hatari.
Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka naye alikuwa ametoa wito wa kuondolewa kwa maafisa wa polisi katika sehemu mbali mbali za jiji la Nairobi.
Alisema haikuwa rahisi kwake kufika katika jumba la KICC kwa shughuli ya leo na akashangaa ingekuwaje iwapo ingefanyika katika ikulu ya rais.
Haya yanajiri muda mfupi baada ya viongozi hao kushuhudia kutiwa saini kwa mswada wa marekebisho ya tume ya uchaguzi na uratibu mipaka nchini IEBC katika jumba la KICC na Rais William Ruto.
Marekebisho hayo yalipendekezwa na kamati ya kitaifa ya maridhiano ya kitaifa kwenye ripoti yake kabla ya kupitishwa katika bunge la kitaifa.
Serikali ilikiri vifo vya watu 25 wakati wa maandamano yaliyoongozwa na Gen Z huku tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu nchini KNCHR ikiweka idadi hiyo kuwa 41.
Tume hiyo ya KNCHR ilitangaza pia kwamba wakenya 361 waliachwa na majeraha kutokana na ukatili wa maafisa wa polisi wakati wa maandamano hayo.
Kikao cha kitaifa cha sekta mbali mbali kinatarajiwa kuanza Jumatatu wiki ijayo lengo kuu likiwa kujadili masuala mbali mbali ambayo vijana wa Gen Z wameibua hadi sasa.